2 Corinthians 11

Paulo Na Mitume Wa Uongo

1 aLaiti mngenivumilia kidogo katika upumbavu wangu! Naam, nivumilieni kidogo. 2 bNinawaonea wivu, wivu wa Kimungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Al-Masihi kama mabikira safi. 3 cLakini nina hofu kuwa, kama vile Hawa alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Al-Masihi. 4 dKwa sababu kama mtu akija na kuwahubiria Isa mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au kama mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au Injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi. 5 eLakini sidhani ya kuwa mimi ni dhalili sana kuliko hao “mitume wakuu.” 6 fInawezekana mimi nikawa si mnenaji hodari, lakini ni hodari katika elimu. Jambo hili tumelifanya liwe dhahiri kwenu kwa njia zote.

7 gJe, nilitenda dhambi kwa kujishusha ili kuwainua ninyi kwa kuwahubiria Injili ya Mungu pasipo malipo? 8 hNiliyanyang’anya makanisa mengine kwa kupokea misaada kutoka kwao ili niweze kuwahudumia ninyi. 9 iNami nilipokuwa pamoja nanyi, nikipungukiwa na chochote, sikuwa mzigo kwa mtu yeyote, kwa maana ndugu waliotoka Makedonia walinipatia mahitaji yangu. Kwa hiyo nilijizuia kuwa mzigo kwenu kwa njia yoyote, nami nitaendelea kujizuia. 10 jKwa hakika kama vile kweli ya Al-Masihi ilivyo ndani yangu, hakuna mtu yeyote katika Akaya nzima atakayenizuia kujivunia jambo hili. 11 kKwa nini? Je, ni kwa sababu siwapendi? Mungu anajua ya kuwa nawapenda! 12 lNami nitaendelea kufanya lile ninalofanya sasa ili nisiwape nafasi wale ambao wanatafuta nafasi ya kuhesabiwa kuwa sawa na sisi katika mambo wanayojisifia.

13 mWatu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Al-Masihi. 14 nWala hii si ajabu, kwa kuwa hata Shetani mwenyewe hujigeuza aonekane kama malaika wa nuru. 15 oKwa hiyo basi si ajabu, kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.

Paulo Anajivunia Mateso Yake

16 pNasema tena, mtu yeyote asidhani kwamba mimi ni mjinga. Lakini hata kama mkinidhania hivyo, basi nipokeeni kama mjinga ili nipate kujisifu kidogo. 17 qNinayosema kuhusiana na huku kujisifu kwa kujiamini, sisemi kama vile ambavyo Bwana angesema, bali kama mjinga. 18 rKwa kuwa wengi wanajisifu kama vile ulimwengu ufanyavyo, mimi nami nitajisifu. 19 sNinyi mwachukuliana na wajinga kwa sababu mna hekima sana! 20 tKweli ni kwamba mnachukuliana na mtu akiwatia utumwani au akiwatumia kwa ajili ya kupata faida au akiwanyang’anya au akijitukuza mwenyewe au akiwadanganya. 21 uKwa aibu inanipasa niseme kwamba sisi tulikuwa dhaifu sana kwa jambo hilo!

Lakini chochote ambacho mtu mwingine yeyote angethubutu kujisifia, nanena kama mjinga, nami nathubutu kujisifu juu ya hilo.
22 vJe, wao ni Waebrania? Mimi pia ni Mwebrania. Je, wao ni Waisraeli? Mimi pia ni Mwisraeli. Je, wao ni wazao wa Ibrahimu? Mimi pia ni mzao wa Ibrahimu. 23 wJe, wao ni watumishi wa Al-Masihi? (Nanena kiwazimu.) Mimi ni zaidi yao. Nimefanya kazi kwa bidii kuwaliko wao, nimefungwa gerezani mara kwa mara, nimechapwa mijeledi sana, na nimekabiliwa na mauti mara nyingi. 24 xMara tano nimechapwa na Wayahudi viboko arobaini kasoro kimoja. 25 yMara tatu nilichapwa kwa fimbo, mara moja nilipigwa kwa mawe, mara tatu nimevunjikiwa na meli, nimekaa kilindini usiku kucha na mchana kutwa, 26 zkatika safari za mara kwa mara. Nimekabiliwa na hatari za kwenye mito, hatari za wanyang’anyi, hatari kutoka kwa watu wangu mwenyewe, hatari kutoka kwa watu wa Mataifa; hatari mijini, hatari nyikani, hatari baharini; na hatari kutoka kwa ndugu wa uongo. 27 aaNimekuwa katika kazi ngumu na taabu, katika kukesha mara nyingi; ninajua kukaa njaa na kuona kiu; nimefunga kula chakula mara nyingi; nimehisi baridi na kuwa uchi. 28 abZaidi ya hayo yote, nakabiliwa na mzigo wa wajibu wangu kwa makanisa yote. 29 acJe, ni nani aliye mdhaifu, nami nisijisikie mdhaifu? Je, nani aliyekwazwa, nami nisiudhike?

30 adKama ni lazima nijisifu, basi nitajisifia yale mambo yanayoonyesha udhaifu wangu. 31 aeMungu na Baba wa Bwana Isa, yeye ambaye anahimidiwa milele, anajua ya kuwa mimi sisemi uongo. 32 afHuko Dameski, mtawala aliyekuwa chini ya Mfalme Areta aliulinda mji wa Dameski ili kunikamata. 33Lakini nilishushwa kwa kapu kubwa kupitia katika dirisha ukutani, nikatoroka kutoka mikononi mwake.
Copyright information for SwhKC